MPIGANIAJI wa
ukombozi wa pili Koigi Wa Wamwere Jumatatu alimtaka rais mstaafu Daniel
Moi kuomba familia ya marehemu Kenneth Matiba msamaha kwa mateso
aliyopitia ndani ya uongozi wake, huku wazee wa Bonde la Ufa wakiitaka
serikali kumzika kishujaa kama alivyozikwa Nelson Mandela.
Bw Wamwere alisema kuwa kifo cha Bw Matiba
kilitokana na shida za kiafya alizopata wakati alipofungwa bila hukumu,
na mateso aliyokumbana nayo akiwa jela.
Mbunge huyo wa zamani wa Subukia alimtaka
Mzee Moi kuwa shupavu na kuiomba msamaha wakati taifa likiomboleza kifo
cha kiongozi huyo, akisema ujumbe wa rambirambi haungetosha.
Alimtaja Bw Matiba kuwa kiongozi
aliyejitolea kupigania Kenya huku akiitaka serikali kukiri makosa ya
uongozi wa mbeleni mbele ya umma kama namna ya kuonyesha kufurahia
matunda aliyopigania marehemu Bw Matiba.
“Ninatarajia kuwa siku zijazo wakati taifa
likiomboleza, mzee Moi atapata ushupavu wa kuomba familia ya Matiba
msamaha, mbali na kutuma rambirambi kwani ni kutokana na kifungo
alichopata wakati wa Moi na mateso yaliyofuata vilivyompa magonjwa
ambayo alirudi nyumbani nayo na kufa baadaye,” Bw Wamwere akasema.
Mwanasiasa maarufu katika vita vya ukombozi wa Kenya kutokana na utawala wa rais mstaafu Daniel Moi, marehemu Kenneth Matiba
Kulingana na Bw Wamwere, mateso waliyopata
viongozi waliofungwa bila kuhukumiwa yalikuwa mengi na machungu,
yakiwemo kunyimwa matibabu na kutengwa kando na watu.
“Kutengwa kando na watu kwa saa 23 na nusu
kila siku ni uchungu, ni kutengwa kikamilifu na hata unapougua haupewi
huduma,” akakumbuka mbunge huyo wa zamani wa Subukia, ambaye pia aliwahi
kufungwa kifungo sawa.
Kwa upande mwingine, wazee wa kutoka Bonde
la Ufa wakiongozwa na mwenyekiti wao Gilbert Kabage waliitaka serikali
kujitwika mzigo wa kumzika mzee Matiba, huku wakisisitiza kuwa marehemu
anapasa kuzikwa kishujaaa kama alivyozikwa rais wa kwanza wa Afrika
Kusini Nelson Mandela.
“Kushikwa na kufungwa kwake ni baadhi ya
mambo yaliyoudhi, lakini matunda yake tumeyaona kama taifa. Marehemu
anafaa kuzikwa kishujaa kama Bw Mandela kwani pia naye alipigania Uhuru
wa wakenya kutoka kwa wakenya wakoloni na matunda yake tunayaona,”
akasema mzee Kabage.
“Mipango ya mazishi inafaa kuwa jukumu la
serikali kama njia ya kukiri kuwa ilikosea kwa kumtesa, na kufurahia
shujaa wa taifa letu,” Bw Kabage akasema.
Moi aombe familia ya Matiba msamaha kwa mateso – Koigi Wamwere
Reviewed by Unknown
on
April 18, 2018
Rating: 5
No comments: