Pwani Ni Kenya


Nyali MP, Mohammed Ali
Enyi wana-si-sasa wa pwani maana mmekuwa tena sio wanasiasa. Kabla muanze kutupiga mnada wapwani eti Pwani sio kenya anzeni kwa kuzoa taka, ajira kwa watoto wetu, vita dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya, malizeni ubinafsi na wizi wa mali ya umma, jengeni shule ili watoto wetu wapate elimu ya kisasa, tumieni pesa za umma kwa miradi na maslahi ya wapwani, acheni ukabila, acheni ubaguzi, punguzeni leseni kwa manufaa ya wafanyabiashara wadogo, ekezeni kwa biashara na ukulima, heshimuni mnaowaita wabara kwani sote ni sawa mbele ya macho ya mwenyezi Mungu, saidieni vichuzi wote mnaowatumia kama chambo kwa kuwapa ajira badala ya shilingi mia mbili kutusi watu na kupiga domo, kuweni na utu na zaidi ya hayo muabuduni Mwenyezi Mungu. Mkitekeleza haya njooni sasa mtueleze mambo mengine! Kwa sasa hamna la kujigamba wala kuwafanya wapwani kufuata ajenda zenu zisizowafaa. Mmewafanya wapwani kuwa mateka ndani ya ardhi yao kwa sababu kila kitu kina jina lenu. Ukitaja ardhi jina lenu halikosi, ukitaja zabuni, biashara, ufisadi, dhulma, ukiukaji wa haki za binadamu na mambo mengine ambayo hayawezi tajika. Acheni kibri na chuki! Wapendeni wenzenu kwa kuwasaidia, kuwaelimisha na kupanua rasilimali ya pwani. Hizi ndoto zenu za kutaka kujitenga ili mzidi kuwanyonya wapwani damu au kutumia semi hizo kama chambo cha kujinufaisha na familia zenu komeni. Wakati MRC walisema pwani si kenya mliwakashifu na kuwakejeli huku serikali ikiwaponda vilivyo. Mamnuazi alijipata kubanwa, mliwakimbia na kuwaacha peke yao kabla ya Gavana wa Nairobi sasa Gedion Mbuvi Sonko kuingilia kati na kuwatolea dhamana. Wakati huo nyinyi viongozi mliwaona kama kero na watu wasiopenda amani. MRC walisukumwa na shida, dhulma na kutaka haki zao kama wapwani. Hawakuwa na chama ila haki. Mlinyamaza wakiteseka kisha leo mwaja na kauli mbiu yenyu ya kunyonya damu za watoto wetu maana hiyo tu ndio imesalia. Bahari mnaikausha kwa kujenga bandari zenu, nyumba na biashara zenu kisha mwatudang’anya eti pwani si kenya. Leo nawaambia pasi na woga kuwa pwani ni Kenya na itasalia kuwa kenya. Tulisalitiwa na serikali ya uongozi wa kwanza kwa kufanya maelewano na serikali ya Sultan wa Zanzibar. Maelewano ya miaka mia moja. Kizazi baada ya kila kizazi ikaingia na kuendeleza usaliti huu. Nyinyi wapya mmeendeleza usalitu huu kwa mpigo. Mnataka jamii ya Wakamba, Wamasai, Wakuria, Wakikuyu, Wameru, Wakisii, Waluhya, Waembu, Wamasai, Wasamburu, Waturkana
miongoni mwa wengi waliooana na kuzaliwa hapa pwani waende wapi? Mnajua maana ya kujitenga? Mnajua uongozi unaofaa kujitenga? Hakika hamjui ndio maana mnaona kujitenga ni kama kuuza kaimati. Iwapo vigogo kama marehemu Ronald Ngala, Juma Boy, Karisa Maitha, Robert Matano, Mekatilili Menza, Sharrif Nassir, Mohamed Bahariz, wangekuwa hai angalau tungelifikiria jambo hilo kwa haraka kwa maana wao walikuwa na doa ya uongozi. Waliwapenda wapwani na kujituma zaidi kuwasaidia, walitupigania na kutusikiza, pwani ilikuwa safi na mkoa wa kuheshimika, tulikuwa na sifa nzuri kote nchini, tulipendana na kuheshimiana, tulishikamana na kuwa na umoja kabla ya kizazi hiki kipya kuingia na kuanza kutugawanya, kutuibia na kuekeza katika ujinga badala ya elimu. Regesheni mali ya umma kabla ya kufoka kwa ajili ya matumbo yenu, regesheni heshima na dini, acheni unafiki kwa maana hii ndoto yenu ni ndoto ya mateja. Ndoto ya kutafuta senti za dawa za kulevya kila baada ya sali moja. Kwa taarifa yenu Pwani itasalia kuwa Kenya. Tunachotaka kumaliza pwani ni ujinga wa kuzaliwa nao na akili ndogo kutaka kutawala akili kubwa. Hii ndio kauli yangu leo, nikifa kesho. Ashakum si Matusi!

Mohammed Ali ni Mbunge wa Nyali na Mwanahabari Mpekuzi
Kuwasiliana naye: rasmohaanothermoses@yahoo.com, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu, Instagram: @mohajichopevu
Pwani Ni Kenya Pwani Ni Kenya Reviewed by Unknown on November 17, 2017 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.